25.12.2018: KUNA WATU WANAJIITA WAKRISTO AU WALOKOLE LAKINI MATENDO YAO NA TABIA ZAO HAZIENDANI NA UKRISTO AU ULOKOLE.


Leo ni siku nzuri ambayo Yesu Kristo amezaliwa na kuchukua dhambi zetu. Muulize mwenzako, “Yesu wako yuko wapi? Yesu umemuacha wapi? Ikiwa ni siku ya 25.12.2018 ambayo ni tarehe ya kukumbuka kuzaliwa kwa Yesu Kristo kwahiyo tunatakiwa kutambua kuwa Yesu kazaliwa lakini Yeye ni Emmanuel Mungu pamoja na wanadamu. Yesu Kristo anataka kukaa na wewe, hataki umuache kanisani peke yake. Ukisoma Mathayo 2:41-51 utaona wazazi wa Yesu hawakumuelewa Yesu Kristo kwani Yesu Kristo alipomaliza Pasaka aliendelea kukaa Hekaluni akisikiliza Neno la Mungu, akijifunza na akiuliza maswali katikati ya walimu na watu waliokuwepo humo hekaluni. Wazazi wake Yesu wakaondoka na hawakujua kuwa wamemuacha Yesu Kristo hekaluni, wakaenda mwendo kama wa kutwa nzima na hawakumuona Yesu Kristo akiwa pamoja nao. 
Katika maisha ya leo watu wengi wanasema wao ni Wakristo au walokole lakini ndani yao sio Wakristo wala hawana ulokole, wanajikuta wamemuacha Yesu kanisani na wanaendelea na mambo yao ya kidunia kama kawaida, ila wanapopatwa na magumu wanarudi kanisani wakihitaji kuombewa. Ninawapa pole watu wanaokaa mbali na Yesu Kristo kwa maana wanakosa mambo mema mengi kutoka kwa Mungu. Ninakuomba Krismasi hii tembea na Yesu kila mahali. 

WATU WENGI UKRISTO WAO NI MBELE ZA WATU LAKINI WAKIWA PEKE YAO WANAFANYA MAMBO YA OVYO OVYO 

Krismasi maana yake ni kutembea na Yesu Kristo kwa maana Yeye alishuka kwaajili yako. Usimuache Yesu Kristo pembeni eti kwasababu watu hawakuoni. Watu wengi Ukristo wao ni mbele za watu au mbele ya mchungaji . Utashangaa baadhi ya Wakristo ukiwakuta maeneo fulani wanavua Ukristo wao lakini wakiwa mbele ya Mchungaji wanavaa Ukristo wao na kuanza kuongea maneno ya upole ya kinafiki. Kama Mtumishi wa Mungu Bishop Dr. Gertrude Rwakatare ninasema, “Unafiki hatutaki bali tunataka Krismasi Yesu Kristo atembee na wewe.” Kama umeamua kumtumikia Yesu fanya kwa uaminifu na sio kutudanganya na kufanya wokovu kama kivuli cha kufanya maovu yako. 


USIMUONEE AIBU YESU KRISTO KWANI NAYE ATAKUONEA AIBU MBELE ZA MUNGU. 

Unatakiwa kukijivunia kuwa na Yesu Kristo, unapaswa kumtangaza Yesu Kristo bila ya aibu yoyote. Yesu anasema, “Atakayenionea aibu mbele za watu na mimi nitamuone aibu mbele za Baba yangu.” Anaendelea kusema, “Ukikubali na kutii utakula mema ya nchi.” Kwahiyo kama Mkristo kazi yako ni kumfuata tu huyu Yesu Kristo kwani ni rafiki wa karibu katika maisha yako, ni ndugu kuliko ndugu yako, yuko karibu kuliko nguo uliyoivaa. Yesu Kristo yupo na wewe kipindi cha shida na raha, yupo wakati wa furaha na huzuni. 


USIMUWEKE YESU KRISTO KAMA “SPEAR” TAIRI. 

Jiulize; “Yesu wako umemuacha wapi?” Wengine Yesu wao ni kama “spear” tairi. Utakuta mtu anamtafuta Yesu Kristo mpaka awe na shida. Akiwa na shida utakuta anamkimbilia na mchungaji wake na kusema, “Ninaomba ufunge na kuomba kwaajili yangu kwani nina majaribu.” 
Nami kama mtumishi wa Mungu Bishop Dr. Gertrude Rwakatare, watu wa namna hii wakija kwangu huwa nawajibu, “Nani akufungie na kukuombea, wakati kipindi unakula raha hukuweza kunishirikisha? Nami sitafunga na kukuombea bali funga na kuomba mwenyewe, mtafute Yesu mwenyewe kwasababu mimi kama mtumishi wa Mungu nilishakuonyesha Yesu alipo.”
 Kama watumishi wa Mungu tumemfundisha huyo mtu jinsi ya kufunga na kuomba lakini yeye hataki kufanya, tumemfundisha kutoa fungu la kumi lakini yeye hatoi. Mtu kama huyo akipatwa na tatizo utaona anakuja mbio kwa wachungaji na kusema, “Mchungaji naomba unisaidie, kule kazini kwangu wanapunguza watu, ninaomba jina langu lifichwe na damu ya Yesu Kristo ili lisionekane nisije nikapunguzwa kazini.” Na mimi kama mtumishi wa Mungu kwasababu hutii unachoambiwa, basi ukija ninakuambia, “Jina lako lionekane wala lisifichwe kwa damu ya Yesu Kristo, kwasababu huna ulinzi wa Mungu kwa kutofanya maombi wala kutoa fungu la kumi.” 
Ninarudia tena kusema, “Usifanye Yesu “spear” tairi, lazima Yesu Kristo umbebe kila mahali.” Huu sio wakati wa kumchezea Mungu wetu kama mjomba wako, unamfanya Mungu kama mfanyakazi wako au chombo cha kutumika baada ya kuona yamekushinda. Unatakiwa kumheshimu Mungu wetu kwa kutii yale anayokuagiza kupitia watumishi wake na kuyafanya yale yote unayoyasoma katika Biblia yake Takatifu ili siku moja ukikumbwa na mabaya uweze kusaidiwa. Mungu akusaidie sana. 


MAMA ALIYEKUWA AKIJIITA AMEOKOKA AIIBIKA PALE WACHUNGAJI WAKE WALIVYOMTEMBELEA BILA TAARIFA. 

Siku moja nilikuwa ninaenda mahali nikiwa nimeongozana na watu kadhaa. Tukiwa njia nikashikwa kiu ya maji. Nikajaribu kuongea na wenzangu niliokuwa nao nikasema, “Ninakumbuka mahali fulani kuna mama mpendwa wa Mungu, ngoja tuingie mahali pale tunywe maji.” Tulipofika eneo lile tukaulizia watu au majirani wa pale ili watusaidi kutuonyesha yule mama anaishi. Nikauliza, “Je, mnamfahamu mama mmoja yuko hivi na hivi mlokole anaishi maeneo haya?” Wale watu wakatujibu, “Tunamfahamu”. 
Wakatuuliza swali, “Kwani kwa yule mama ameokoka?” Wakasema, “Yule mama hajaokoka kabisa.”  Tukawauliza tena wale watu, “Mnamjua lakini tunayemsema?” Tukataja sifa zak yule mama. Wale watu wakasema, “Ndio ni huyo huyo mama tunamfahamu, ila ngoja tukuitieni aje.” Baadae tukaja kugundua kuwa yule mama alikuwa hainui bendera ya Yesu Kristo mtaani kwake wala hasemagi ameokoka kazini kwake. Tulishangaa sana kuona majirani zake wanamjua kwa tabia fulani na sisi tunamjua kama mlokole mwenzetu. 
Kama Mkristo unatakiwa kuinua bendera ya Yesu Kristo kila mahali, unatakiwa kujitangaza kuwa umeokoka ili watu wakuelewe. Unatakiwa kutangaza msimamo wako wa wokovu ukiwa sokoni, kazini kwako, hospitalini unakofanya kazi, mtaani kwako. Watu mpaka siku ya shida ndipo wanamtaka Yesu Kristo. Yesu anataka kukuona wewe macho kwa macho, yuko karibu na wewe kukusaidia lakini wewe unajitenga naye. Kuna watu mitaani kwao hawajulikani kwasababu hawainui bendera ya Yesu Kristo. 
Baadhi ya watu wanapokuwa kanisani wanajifanya Watakatifu sana na wanyenyekevu mbele za BWANA lakini wakitoka nje ya eneo la kanisa wanageuka kuwa simba, tabia zao zinakuwa kama za watu wasiomjua Mungu, wasiokoka na wasio na hofu ya Mungu. Wokovu wao unakuwa wa moto wanapokuwa kanisani lakini wakiwa nje ya kanisa wokovu wao unapoa na kuwa wa baridi. Huu si wakati wa kumchezea Mungu wetu na kumfanya ni “spear” tairi. 
Mungu wetu ni wa thamani sana kwani yeye ndiye aliyekuumba wewe ambaye unajifanya kidume na unashindwa kumtumikia Mungu wako. Kumbuka siku ya kutoka hapa duniani, Mungu wetu atakutema kama matapishi kwasababu hukumtumikia ulivyokuwa duniani wala kuinua bendera yake. Maisha yako ya duniani yalikuwa ya kumuudhi na kumdhalilisha Mungu wetu, ulikuwa ni mtu usiyekuwa na huruma na upendo kwa Mungu. Kila wakati ulikuwa ni mtu wa kumuumiza Mungu wetu. Kutokana na tabia zako mbaya na matendo yako mabaya, Mungu wetu atakutupa motoni uungue milele Amua sasa kumtumikia Mungu wako . 


BISHOP DR. GERTRUDE RWAKATARE APATA MUUJIZA WA KUPANDA GARI LA MATAJIRI DUNIANI BAADA YA KUKIRI HADHARANI KUWA AMEOKOKA NA ANAMPENDA YESU KRISTO. 

Siku moja tulienda Marekani na tulichaguliwa wanawake 23, Uganda mmoja, Tanzania nikawa mimi Bishop Dr. Gertrude Rwakatare peke yangu na wengine kutoka mataifa mengine. Tukaenda kukutana kwenye mkutano mkubwa wa viongozi New Jersey – New York . Tukiwa pale New York, tukisubiria “dinner” sasa wakati wakitengeneza “dinner” yetu ambayo ilikuwa na vyakula vingi vyenye manjonjo mengi, mashamsham, vimwengu mwengu vya kuweza kuvutia na kuwapa hamu ya kula chakula wageni wa mataifa yote waliokuja kwenye huo mkutano mkubwa. 
Sasa kikikafika kipindi cha kujitambulisha, kwahiyo kila mtu aliweza kujitambulisha jina lake, mahali anapotoka na kazi yake. Ilipofika zamu yangu nikasema, “Mimi ninaitwa Dr. Gertrude Rwakatare kutoka Tanzania, ninamshukuru Mungu kwa kuwa na cheo hiki na hiki lakini zaidi yote nimeokoka, ninampenda Yesu kama BWANA na mwokozi wangu.” Nakumbuka kipindi hicho nilikuwa bado sijawa mchungaji wala Askofu ila nilikuwa mzee wa kanisa tu. Nilipotamka jina langu na sifa zangu watu wakapiga makofi sana. 
Tulipomaliza kikao yule aliyeandaa kalamu na vyakula mbalimbali kumbe mwenyekiti wake ni mlokole. Nilipomaliza tu kujitambulisha yule mtu akaja na kuniambia, “Sister on Sunday I am going to pick you and worship with us in our church. We will like to hear your testimony.” Akasema, “Tungetaka kusikia ushuhuda wako mama yetu kwasababu hata mimi nimeokoka na ningetamani kukuletea gari moja moja kubwa sana lije kukuchukua.” 

Nikakubaliana naye na tukaangana. Siku ya Jumapili likaja gari kubwa sana ambalo sijawahi kupanda maisha yangu yote. Gari hilo ni aina ya “Limozini” ambalo ni gari refu sana, gari la waheshimiwa. Ndani ya hilo gari kuna meza, TV, choo, kitanda, friji na kila kitu. Lile gari likaja na waliomo kwenye gari wakasema, “Welcome mama Gertrude from Tanzania.” Nikiwa natoka kwa ujasiri huku nikiwa na Biblia yangu kuelekea kwenye gari akatokea mama mmoja wa Ki-Nigeria akaenda kumwambia yule mtu aliyekuja na lile gari la kifahari kunichukua, akasema, “Me too I’m saved.” 

Nikashangaa sana nikasema kimoymoyo, “Kwanini haukusema wakati nikitoa ushuhuda mara ya kwanza, gari imekuja kwaajili yangu halafu na yeye anajibembeleza eti ameokoka. Wakati mimi ninajitambulisha kwa mara ya kwanza sikumficha huyu Yesu Kristo wangu, mimi nilitembea na Yesu, nilimtangaza Yesu, gari hili ni langu.” Nikasema, “Is Too late” 
Na siku za mwisho kuna watu watakaposahaulika, watapokatazwa na Mungu kwasababu walimuone aibu Yesu Kristo wakiwa duniani, vinono kutoka kwa Mungu watavikosa. 
Basi Yule dada M-Nigeria naye akachukuliwa huku macho yake yakifanya kopokopo kwasababu alikuwa na aibu. Huyu M-Nigeria alipata nafasi ya kuondoka na mimi baada ya kuwmwambia yule mtu aliyekuja kunichukua na na gari la kifahari kwa kusema, “My friend from Nigeria is also born again.” Wale watu wakamsalimia kwa kutomchangamkia, tofauti na walivyonichangamikia mimi. Wale watu wakamsalimia yule M-Nigeria kwa kutomchamkia wakisema;, “Ooh sister how are you?” Wakasema, “We have only one testimony from one person and is Gertrude Rwakatare. 
Yule M-Nigeria alijisikia vibaya na kuona kweli alizamia safari ambayo haikuwa yake. Kwahiyo kila mahali tembea na Yesu ndipo utaona baraka zake. 


Mhubiri: Bishop Dr. Gertrude Rwakatare.
Kanisa la Mlima wa Moto Mikocheni “B” 

Tarehe: 25.12.2018 

Ujumbe: Kuzaliwa Kwa Yesu Kristo 







































































Comments