13.01.2019: HAPPY KWAYA WATUBARIKI KATIKA KONGAMANO LA SIKU MOJA LA UREJESHO WA SHEHENA.


BWANA apewe sifa. Ninapenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru watumishi wa Mungu Happy Kwaya na Joybringers Kwaya kwa kazi ya BWANA waliyoifanya siku ya Jumapili 13.01.2019 katika Kongamano la Siku Moja la Kurejesha Shehena ya ajira, kazi, biashara, afya, mahusiano,amani katika ndoa n.k iliyofanyika katika kanisa la Mlima wa Moto Mikocheni "B". 



Hakika tumebarikiwa sana na uimbaji wao na jinsi walivyojitoa kwaajili ya kumsifu Mungu aliye juu na kutukumbusha mambo mengi kupitia ujumbe waliokuwa wakituimbia kupitia nyimbo zao. Mungu azidi kuwainua na kuwatunza katika kazi zao, huduma yao, majumbani mwao, afya zao, masomo yao na maisha yao kwa ujumla. 



kama wapendwa wa Mungu tuzidi kuwaombea ili wazidi kutunga na nyimbo mpya kutoka kwa BWANA kwasababu kupitia nyimbo zao tunajifunza, tunaelimishwa, tunakumbushwa, tunaadibishwa, tunapokea upako, tunapokea ujumbe kutoka kwa Mungu, tunainuliwa kiimani n.k. Kwahiyo tuwapo kanisani tunapaswa kuwasikiliza kwa makini waimbaji wetu na kuutendea kazi ule ujumbe wanaouimba katika maisha yetu. Na tukumbuke ya kuwa Mungu wetu mara nyingi huwepo katikati ya watu wanaomsifu kwa roho wa kweli, kwahiyo unapoona watu wanaimba na kumsifu Mungu ni lazima uungane nao ili uweze kupokea muujiza wako kupitia nyukbo za sifa. 



Unapoimba na kucheza unatakiwa kumaanisha na sio kuiga watu au kufuata mkumbo. Mungu wetu huangalia mioyo yetu kama kweli inamsifu na kumwabudu kutoka ndani ya mioyo yetu. Mungu wetu anatamani kukuona unamsifu kwa kumaanisha na sio kuimba ili mradi unaimba wimbo. Muombe Mungu akuongoze unapotaka kumsifu ili unapomsifu na yeye akujibu kulingana na yale maneno unayotamka katika ule wimbo. 



Mungu akubariki sana na ninakukaribisha katika ibada ya Jumapili saa 3 asubuhi hadi saa 8 mchana.



--------------

Bishop Dr. Gertrude Rwakatare
Mlima wa Moto Mikocheni "B"













Comments