02.09.2018: MAMA ASHUHUDIA UNABII WA BISHOP DR. GERTRUDE RWAKATARE WA KUPATA UJAUZITO NA KUJIFUNGUA MTOTO.

Siku ya Jumapili 02.09.2018 muumini wa kanisa la Mlima wa Moto Mikocheni "B" akiwa na mume wake waliweza kushuhudia jinsi Mungu alivyowawezesha kupata mtoto. Ushuhuda huu ulitolewa kwenye ibada ya KUZAA MUUJIZA WAKO, na alikuwa na haya ya kusema, "Bwana Yesu asifiwe, ninapenda kumshukuru Mungu mimi na mume wangu kwa familia yetu kuongezeka na kuongeza muumini mwingine hapa kanisani kwetu Mlima wa Moto Mikocheni "B". 

Nakumbuka kipindi sijapata ujauzito Mch. Prisca Charles wa kanisa la Mlima wa Moto Mikocheni "B" alikuwa akituombea hapa kanisani akisema, "Pokea mtoto, pokea mtoto wa kike, mkazae mapacha." Na mimi nikawa napokea kwa imani.
Nakumbuka mwezi wa tisa mwaka 2017 Bishop Dr. Gertrude Rwakatare akiwa madhabahuni alisema, "Mwezi wa tisa ni mwezi wa kuzaa." Na mimi nikawa napokea kwa imani yale maneno aliyokuwa akitamka madhabahuni akisema, "Nasikia mtoto analia..pokea mtoto wako, naona unanyonyesha..pokea mtoto wako!..." Wakati anaongea hayo yote na mimi nikawa napokea kwa imani. 
Wapendwa, mwezi huo huo wa tisa 2017 nikawa nimepata mimba, namshukuru Mungu sana. Mungu kwa kupitia mtumishi wake Bishop Mhe. Dr. Gertrude Rwakatare ameweza kunipa KICHEKO kwa kupata huyu mtoto. Kicheko nilichopata naomba na wewe unayehitaji mtoto upokee kwa jina la Yesu.
Pia nakumbuka siku ya Ijumaa mwezi wa nne 2018 Bishop Mhe. Dr. Gertrude Rwakatare alifanya maombi maalum kwa wenye UJAUZITO, na mimi tayari nilikuwa nimeshapata ujauzito na nimechoka nikawa nashindwa kuja kanisani kutokna ana uchovu wa ujauzito. 
Siku moja bibi yangu akanipigia simu na kuniambia, "Nasikia Praise Power Radio 99.3fm wanatangaza kuwa Mlima wa Moto Mikocheni "B" kuna maombi ya wajawazito. Nilipofungulia redio, nikasikia wachungaji wakisisitiza sana wajawazito kutokosa kushiriki maombi. Nikamuomba mume wangu siku ya Jumanne anilete kanisani ili niombewe. Nakumbuka ilikuwa ni saa 12 jioni na tukawa tumeambiwa kuja na khanga kwaajili ya kushikia mtoto kwa imani. 
Tukiwa kanisani tukaomba sana, na wiki iliyofuatia siku ya Ijumaa hali yangu ikawa mbaya kutokana na presha kupanda. Tukaanza maombi na mume wangu na baadae tukaelekea hospitalini. Nikiwa thieta nikaushika mkono wa daktari kabla hajaanza kazi yake ya kuzalisha na nikasema, "Nautakasa mkono wako wewe daktari kwa damu ya Yesu". Baada hapo nikajifungua mtoto ambaye ndio huyu hapa. Namshukuru sana Mungu.

Nakumbuka Bishop Dr. Gertrude Rwakatare alikuwa akituambia ya kwamba "Kuwa na mimba sio kwamba umepata mtoto. Wewe njoo kwenye maombi kwani unaweza kuwa na mimba na mtoto akafa wakati wa kujifungua."


Namshukuru sana Mungu na Bishop wangu pamoja na Mch. Prisca Charles kwa maombi yao na sasa nina mtoto. Mungu awabariki sana














Comments