31.12.2018: CROSS OVER NIGHT | MKESHA WA KUKARIBISHA MWAKA MPYA. MAHUBIRI YA BISHOP DR. GERTRUDE RWAKATARE YA KUVUNJA LAANA NA MANENO MABAYA ULIYOTAMKIWA NA WABAYA WAKO

BAADHI YA VITU VYA KUMUOMBA MUNGU MWAKA 2019: 

Muombe Mungu akubariki, akupe hatua ya kiroho na ya kimwili, akuinue kiuchumi, akuondolee madeni, akuondolee aibu ya kuchekwa, kudharauliwa. na akupe hatua moja zaidi mwaka 2019
Bishop Dr. Gertrude Rwakatare

USIKU WA KUVUNJA LAANA NA NENO BAYA ULIYOTAMKIWA.

Naomba ukipata nafasi soma Mwanzo 49:1-4 na Kumbukumbu la Torati 33:6. Katika kesha wa leo wa kukaribisha mwaka 2019 yaani “Cross Over Night” ni usiku wa kuvunja laana na maneno mabaya uliyotamkiwa labda na mchawi, adui yako, shangazi yako au watu waliotamka maneno mabaya juu yako. Usiku huu tunaenda kuvunja kila neno baya lililotamkwa juu yako na badala yake tunaenda kutamka neno.

Katika usku wa leo nataka niseme hivi, Usiku wa leo tumemaliza mwaka na tunaanza mwaka mpya. Katika mwaka mzima umepita katika mabonde na milima, furaha na uchungu, mateso na raha, kicheko na machozi. Huwezi kuingia mwaka 2019 na hali ya zamani, ni lazima yale yaliyokutesa niyang’oe.



KUVUNJA LAANA MAANA YAKE NINI?

Laana ni maneno, matamshi yanayoweza kusema na mzazi wako, shangazi yako, adui yako, wachawi, adui zako na kuna watu wengine wanakodi wachawi watamke maneno mabaya juu yako. Huwezi kusema huna adui kwani hata mimba ya tumboni ina adui wake. Utashangaa kuona mimba haijamkosea mtu yeyote lakini watu wana laani tumbo ili lisizae au mimba iharibike, hata barabara iliyonyooka kama haina matuta ina laaniwa na wakazi wa maeneo hayo (utasikia watu waanzisha mgomo wakitaka serikali kuweka matuta barabarani kuepusha ajali), barabara yenye mashimo ina laaniwa sembuse wewe na mimi. 

Unaweza kusema, “Mimi hakuna mtu wa kunilaani”, lakini kumbuka tumetoka vijijini na huko vijini kuna madhabahu za ukoo, kuna matambiko ya mababu na mabibi, maadui wa ukoo, wanakaa wakikutamkia maneno mabaya kutokana na wivu wao wakisema, “Na hata yule kijana anayekaa jijini Dar es Salaam asifanikiwe kabisa, akipata kazi afukuzwe kama mbwa koko. Kwahiyo ni lazmia tuvunje laana zote kwa jina la Yesu. Kila yaliyotamkwa mabaya yasifanikiwe kwetu na yakawarudie wao kwa jina la Yesu Kristo.


INASEMEKANA UCHAWI TANZANIA NI ASILIMIA 8

Kuna siku moja nilikuwa nimekaa na wataalamu fulani kutoka mataifa mbalimbali, tukawa tunataniana. Wataalamu wale wakanambia, “Lakini Watanzania mmezidi sana ushirikina na nyie sio wachawi bali ni washirikia sana, inasemekana. “8 percent of Tanzanians” ni washirikina wakibwa sana. Kama mshirikina halogi lakini anatuma mwenzake au mshirikina mwingine kwa kumkodi ili amulogee au akuloge. Maneno yale yaliniuma sana na nilichukia sana ushirkina kwasababu ni mbaya sana katika jamii yetu.

Katikati yetu kuna watu wametamkiwa maneno mabaya, na wengine wametamkiwa hata na wake zao ili wasifanikiwe kwa kile wanachokifanya. Kama mtumishi wa Mungu ninatengua maneno mabaya uliyotamkiwa na ninakutamkia baraka katika maisha yako. Yale uliyotamkwa mabaya yakawarudie wao katika jina la Yesu Kristo.


MWANAUME AMLOGA MKE WAKE KWASABABU YA UZURI WAKE.

Kuna mume mmoja alimuloga mke wake kwasababu alikuwa mzuri sana, Akamtamkia maneno mabaya akasema, “mke wangu mzuri akipita mbele za watu na hasa wanaume aonekane ananuka kama king’ila na asipigiwe hata mluzi.” Yale maneno mabaya yakatokea kwa mke wake, watu wakaanza kumchukia na hakuna mwanaume aliyeweza kumfuatilia au kumtongoza yule mwanamke mrembo kwasababu alinenewa maneno mabaya na mume wake. 

Kwahiyo usiku wa leo tumetenga kwaajili ya kuvunja laana na maneno mabaya uliyotamkiwa na wabaya wako usifanikiwe kwa lolote, maneno mabaya yanayozuia usiendelee mbele. Maneno unayotamkiwa na wabaya wako mara nyingi hutokea kama hauko vizuri na Mungu wako. Watu wanaotamka maneno mabaya wamejazwa maneno machafu na wakiyatamka yanatokea kwako, kwahiyo unatakiwa kuwa makini na kujikingakwa kufanya maombi ya vita dhidi ya maadui zako. Adui yako anaweza kuwa huyo rafiki yako kipenzi, mume wako, mke wako, ndugu yako, boss wako, mfanyakazi mwezako, housegirl wako au mtu yeyote yule.



BABU AMTAMKIA MANENO MABAYA YA LAANA MSICHANA MZURI ALIYEKATAA KUOLEWA NAYE.

Kuna msichana mzuri kijijini alimkataa babu mmoja aliyetaka kumuoa akasema, “Mimi siwezi kuolewa na mtu mzee kama babu yangu.” Yule babu akamtamkia manenoa mabaya yule msichana mremba akasema, “Uzuri wake uonekane kama makapi, apeperushwe kama makapi yanavyopeperushwa, wanaume wote wamchukie.” Yale maneno yakaumbika kwa yule msichana mrembo. Yule msichana akafikisha miaka 50 bila kuolewa na hakuna mtu aliyemtamkia kuwa anampenda hata kama alikuwa mrembo sana. 
Baada ya kuona haolewi akaona ni vyema kuzaa na mtu asiyempenda akiwa nyumbani yaani bila kuolewa, akaona ni heli apate mtoto tu kuliko kuzeeka bila mtoto. na yule aliyemzalisha hakumuoa kwasababu yule babu alimtamkia maneno mabaya ya laana kwa yule msichana. Yawezekana mahali ulipo umetamkiwa maneno mabaya, huendelei na kazi kutokana na maneno mabaya, wamekutamkia usifanikiwe. Nataka nikutamkie kuwa kwa mamlaka niliyopewa na Mungu nafuta maneno mabaya na laana kutoka kwa watu wasiokupenda na ninakutamkia baraka na mafanikio mwaka huu 2019 na utaolewa.



KIJANA AFUTIWA LAANA YA KUFUKUZWA KAZI.

Kuna mtu mwingine alikuja kwangu analia anasema, “Mchungaji Bishop Dr. Gertrude Rwakatare yaani mimi sijui nina mikosi gani, huu ni mwezi wa tatu sina kazi, nnafukuzwa kazi, na hii ni kazi yangu ya nne lakini nafukuzwa..” Nikamwambia, “Nenda ukajichunguze, labda unafukuzwa kutokana na jeuri yako kazini, au unachelewa kazini, hujali mabosi wako au mzembe kazini au huna juhudi kazini. 
 Lakini kama zitakuwa sio hizo sababu za wewe kufukuzwa kazi na kukosa kazi basi njoo nikuombee.” Yule mtu baada ya kujichunguza nyumbani kwake akaja kwangu tena na kunieleza yote, nikamuombea akapata kazi na sasa yuko kazini na ni mwaka wa tatu sasa.



HADITHI YA RUBENI KULALA KITANDANI NA MAMA YAKE MDOGO

Ukisoma katika Biblia utaona Yakobo alikasirika sana kwasababu ya mtoto wake Rubeni kutembea au kulala na mke wa Yakobo mdogo. Ukisoma katika Biblia utaona Yokobo alikuwa ameoa mtu na mdogo wake ambao ni Leya na Recho. Recho alipokawia kuzaa akasema, “Chukua mjakazi wangu”, na vile visichana vikaolewa na mzee. 
Ruben akampenda mama yake mdogo akalala naye, na baba yake aliposikia alikasirika sana akamlaani na kumtamkia maneno mabaya, akasema, “Rubeni japokuwa ni mzaliwa wangu wa kwanza, una nguvu, una uwezo, ninakupenda lakini kwasababu uliruka na kupanda kitanda cha mama yako mdogo na ukalala naye, ninakulaani na ninakuambia ya kuwa kufa lazima utakufa, utakuwa mdogo kuliko ndugu zako hata kama wewe ni mkubwa, utadharauliwa na kila mtu.
 Maneno aliyotamkiwa Rubeni yakamtokea katika maisha yake. Ruben kiila anapojitahidi kwenda mbele kimaendeleo anarudishwa nyuma, akaambukizwa roho ya utelezi, hawezi kwenda mbele, kila akijitahidi anateleza anarudidi nyuma kwasababu alilaaniwa na baba yake. Lakini Musa akaona hali hiyo kwa Rubeni akasema, “haiwezekani, mimi ni mtumishi wa Mungu nitatengua kila maneno aliyonenewa Ruben,. Basi Musa akapunguza yale makali ya maneno aliyonenewa Rubeni akasema, “Rubeni utaishi lakini watu wako watakuwa wachache.”


Leo Musa wa kizazi hiki ni mimi Bishop Dr. Gertrude Rwakatare, ninatengua kila neno baya walilokutamkia ili lisiwe nguvu kwako kwa Jina la Yesu Kristo, walisema watoto wako hawataolewa, mimi ninatengua kwa Jina la Yesu Kristo , watoto wako wataolewa kwa jina la Yesu, walisema hutaishi, utauguaugua hadi ufe, mimi kama Musa wa kizazi hiki ninatengua maneno yao kwa Jina la Yesu Kristo, na hautakufa bali utaishi na utasimulia matendo makuu ya Mungu. 
Ninaongea na wewe waliokutamkia maneno kuwa ukipata kazi utafanya miezi michache ili uonje tu mshahara na baada ya hapo ufukuzwe kazi, ila mimi kama mtumishi wa Mungu ninatengua mananeo yao na ninakutamkia Baraka, ninasema utapata kazi, utaendelea na kazi yakomkama kawaida, utastaafu ukiwa mzee. Waliokutamkia hutazaa watashangaa unashika mimba na unazaa mtoto mzuri kabisa. 

Kuna wengine wametamkiwa kuwa koo zao zina balaa, mikosi, matasa yaani koo za watu wasiozaa lakini leo kwa damu ya Yesu ninasafisha laana hizo na maneno mabaya kwa damu ya yesu Kristo, ninaondoa mikosi, uchawi, manuizo, mikosi na kila manuizo walionuiza kwako ili usifanikiwe kimaendeleo, kiroho, kimwili, kiafya, kihuduma, kimasomo, kimahusiano, kibiashara n.k.hayana nguvu tena kwa Jina la Yesu Kristo. Wale waliotegemea kukuona unaabika wataabika wao na kazi zao zitayumba kwa Jina la Yesu. Huu sio wakati wa kuonea wivu na kuharibiana maisha. Kila anayekuwazia mabaya, yakamrudie yeye mara mbili yake.



MWAKA 2019 NI MWAKA WA ONGEZEKO NA MAFANIKIO
Nikiwa mtumishi wa Mungu Bishop Dr. Gertrude Rwakatare ninatamka rasmi kuwa huu ni mwaka wa Ongezeko na Mafaniko kwako. Kama huu ni mwaka wa mafanikio ni lazima ukang’are, ukapokee baraka kwa jina la Yesu. Kama ulikuwa ukipata milioni 10 kwa tamko langu kama mtumishi wa Mungu unaenda kupata million 40, unaenda kupata ongezeko la mtaji. Mtu wa milioni 10 utapata mtaji wa milioni 20 kwa Jina la Yesu.

Tunasoma katika Biblia kuwa wana wa Israel waliongezeka na walipoongezeka walikuwa ni wengi mno. Nami ninasema na wewe utaongezzeka na mali zako zitakuwa nyingi mno. Mashamba yako, mifugo yako, utajiri wako utakuwa mwingi mno kwa Jina la Yesu Kristo. Mwaka huu 2019 ninaamuru maendeleo kwako, uende ukajenge majumba kama njugu, ninaamuru ununue magari mengi yajae kama box za biskuti. 

Ninaona mtaa ukijaa majumba ya wana Mlima wa Moto kwa Jina la Yesu, ninaona magorofa, majumba ya kupangisha na ya watu binafsi. Kama unaamini pokea majumba, maongezeko ya magari kwa jina la Yesu. Ninaamuru ongezeko juu ya biashara yako, biashara yako ikaoongezeke mara dufu, vyeo kazini, safari za Marekani , China, Dubai, mikoani zikushukie kama mvua ya mawe. Pokea safari zenye pesa pokea kwa Jina la Yesu. Kama ulipunguzwa mshahara ninawaamuru mabosi wako wakaongeze mshahara kwako, kama walificha barua zako za “promotion” ili upate vyeo ninaamuru jeshi la malaika linalotutumikia sisi watoto wa Mungu liende kila ofisi kufichua barua hizi.

Kama mwaka 2018 ulikuwa ni mwaka wako wa magonjwa naamuru uponyaji , huzuni ninaamuru furaha, shida ninaamuru raha, kuchukiwa ninaamuru kupendwa, kudharauliwa ninaamuru kuheshimiwa, kusengenywa ninaamuru kutosengenywa, ukichekwa ninaamuru heshima na kuthaminiwa, uking’ong’wa ninaamuru kupendwa, pia mwaka huu ninaamuru baraka, heshima, mafanikio katika akaunti yako ya benki, ghala lako na pesa zako zionekana nyingi kwa Jina la Yesu Kristo. 

Sasa muende mkalime mashamba makubwa, mkafanye kazi kubwa kubwa, mkapokee miujiza mikubwa mikubwa, mkang’are na kupendeza, majina yenu yawe sukari na chumvi kwa mabosi wenu na kila mnalofanya kwa kazi ya mikono yenu likafanikiwe kwa ukubwa. Nasema, pokea kibali, upendeleo na ongezeko kwa jina la Yesu. Ninang’oa kila uchawi, ndumba waliokutupia, katika jina la Yesu. Na sasa uko huru, pokea kufunguliwa kwa jina la Yesu

MAOMBI YA KUMSHUKURU MUNGU KUINGIA MWAKA 2019

Sema Ee, BWANA Yesu, ninakushukuru, umenivusha mwaka 2018 na umeiniingiza mwaka 2019. Ee Mungu wangu ninaomba unisaidie. Ninaomba uniondolee mateso, aibu, madeni, kushindwa katika Jina la Yesu Kristo. Ninajivika hatua ya mafanikio, ya kubarikiwa, ya utajiri, ya afya njema kwa Jina la Yesu. Amen

-------

Mhubiri: Bishop Dr. Gertrude Rwakatare.

Mahali: Mlima wa Moto Mikocheni "B"

Tarehe: Jumatatu 31.12.2018

Tukio: Cross Over Night / Mkesha wa Mwaka mpya 2019


















Comments