06.01.2019: TAARIFA MBAYA KWA MADHABAHU ZA KISHETANI ZILIZOKO VIJIJINI DHIDI YA WATU WA MIJINI

KUNA WATU KIJIJINI KWAKO WANAKUTAFUTA WAKUHARIBIE MAMBO YAKO.

Ukisoma kitabu cha Nehemia 6:2-4 kinasema, “Sanibalati na Geshemu wakatuma wajumbe kwangu, wakasema, Njoo, tukutane huko vijijini katika nchi tambarare ya Ono. Walakini wakakusudi kunifanyia mabaya. Na mimi nikatuma wajume kwao, nikasema, Hii ni kazi kubwa ninayoifanya mimi, hata nisiweze kushuka; mbona kazi ikome hapo nitakapoiacha, niwashukie? Nao wakaniletea maneno kama hayo mara nne; nikawajibu maneno kama yale.”



Kwahiyo Sanibalati alikusudia kumuangamiza Nehemia na kazi anayofanya na akutuma ujumbe mara nne, lakini mtumishi wa Mungu Nehemia akapanji yaani akagoma, lakini bado hakuridhika akatuma tena akiwa na lengo lake la kuharibu kazi wanayofanya. Kuna watu wapo kijijini kwako wanatamani sana kukuona unaishi maisha ya taabu huku mjini, kila siku wanakaa vikao wakiwaza ni jinsi gani wanaweza kukuteketeza, kukuangamiza na kukuharibia mipango yako.

Yawezekana ni rafiki zako wa zamani au ndugu zako wa karibu walipo kijijini kwako ambao ndio chanzo cha maisha yako kuwa magumu bila ya wewe kujitambua. Watu hawa wamekuwa wakikunenea maneno mabaya ili usifanikiwe na badala yake upatwe na mabaya. Unajitahidi sana kufanya kazi kwa bidii lakini mafanikio unayopata ni kidogo sana kulingana na kazi unayofanya. Umekuwa ni mtu wa mikosi na balaa katika maisha yako, kila unalofanya halifanikiwi kwasababu kijijini kwako kuna watu wamekutupia maneno mabaya juu ya maisha yako kwasababu ya wivu wao wanapoona uko mjini wakati wao wako kijijini.



Kama mtumishi wa Mungu, ninafunga kila milango yao na njia zao wanazotumia kukuangamiza na ninakufungulia milango ya mafanikio na maongezeko. Ninaharibu mitego yao kwa jina la Yesu na ninaruhusu malaika wa Mungu wakulinde na hao wabaya walioko kijijini kwako wanaotamani kuona maisha yao yanakuwa ya ovyo kama maisha yao. 

Kila wanachokunenea kikawarudie wao na wasifanikiwe kwa kila wanachokifanya kwa Jina la Yesu Kristo. Kuna watu wanajifanya wema kijijini kwako ukikutana nao lakini mioyo yao imejaa chuki, utaona mtu anakusalimia wakiwa na sura za furaha kumbe mioyo yao imepakwa masizi. Leo tunatangaza vita dhidi ya wabaya wako, kila wanachokuwazia kibaya kikatokee katika maisha yao ili wajifunze kuwa wanachokuwazia ni kibaya. Mungu akusaidie mwaka 2019 usipatwe na mabaya kutoka kijijini kwako.

JIHADHARINI NA WANADAMU WABAYA KWANI WAPO KAZINI KUKUTEKETEZA
Mara nyingi adui hatakuacha mara moja kama ukimshinda. Mungu anasema jihadharini na wanadamu kuliko simba kwasababu ukimkwepa simba au tembo mara moja kuja kukutana naye sio leo wala kesho lakini mwanandamu utakutana naye na atakufanyia ubaya, kwahiyo jihadharini na wanadamu kwani sio kila mtu anakuwazia mema. 
Mwanadamu ukimkwepa atakutatufuta mara ya kwanza mpaka mara ya tano ili akupate na akuharibie mambo yako kwasababu ana nia ya kukuharibia kazi yako, ajira yako, biashara yako, ndoa yako, mahusiano yako, furaha yako, afya yako, amani yako n.k kwahiyo atafanya juhudi zote akuangamize.

WAPO WATU WENGI SANA KIJIJINI KWAKO WANAKUWINDA WAKUHARIBIE MAISHA YAKO.
Wapo watu wengi kijijini kwa wanatamani kukuona wewe unayeishi mjini mambo yako yakiharibika. Hawapendi kukuona unaishi mjini kwa raha wakati wao wanahangaika kijijini kwahiyo wanatumia kila njia kukuharibia usifanikiwe katika mihangaiko yako. Na ndio maana nikasema, “Andika jina la kijiji chako ambako umezaliwa, mahali ambako shughuli za kukuangusha zinatendeka bila ya wewe kujua.” 

Unaweza ukawa unaishi jijini Dar es Salaam au mji wowote ule lakini kijijini kwako wako watu wanakunenea mabaya, wanakunuia mabaya juu yako. Utashangaa kijijini kwako Kyela au Tukuyu wanasema, “Kako katoto kanaitwa Mwakitalu kako Dar es Salaam, tunaomba kasifanikiwe.” Kuna watu kijijini kwako wanakusukia mambo mabaya, unashangaa umeanza kazi mara unaachishwa, unajitahidi kufanya kazi lakini haiendi, unaona mambo yako yanaharibika. Vijjini kwetu ndiko kuna madhabahu za kichawi zinazoturudisha nyuma.

Leo tutavunja madhabahu za vijini zinazikuharibia maendeleo yako. Sijui unatoka kijiji gani lakini leo nina neno juu ya kijiji chako. Kuna madhabahu ya uharibifu juu yako inayofanya safari yako ya maendeleo iwe na utelezi, kila unavyojitahidi kwenda mbele hatua sita unateleza na kurudi nyuma hatua saba, maisha yako yanakuwa ya ovyo ovyo hata kama unaishi mjini. Ninaona kuna watu wanaharibu pale kwenye nyumba yenu, wamekuwa wakizika vitu, wakinuiza mabaya, wakisema mabaya juu yako, wanakurudisha nyuma usiendelee mbele.

Watu tunayetoka kijijini mara nyingi tumekuwa tukiona watu wengi wa vijijini macho yao mekundu na inafika kipindi unaogopa kutoka nje ya nyumba yako kwasababu wanakijiji hao wanauchungu na hasira, wanapoona watu na vijukuu vimekuja kijijini vikitokea mjini huku vimevaa vizuri basi wao wanachukia kutokana na wivu wao na roho mbaya; wanapoona umekuja na gari kwenye mji wenu wanachukia na wanatamani gari lako lipate ajali au liharibike kabisa na lisionekane kijijini kwao. Lakini leo nasema kila walichokipnga kibaya kikudhuru kitawarudia wao kwa Jina la yesu Kristo.

WANAKIJIJI WABAYA WALIOKUNENEA MABAYA USIFANIKIWE LEO WATAKIONA CHA MOTO.
Kuna watu wabaya sana wapo vijijini na wamekuwa na mioyo ya ajabu sana dhidi ya watu wanaoishi mijini. Tunatambua asilimia kubwa ya watu tunatoka vijijini na tunakuja mijini kwaajili ya kujitafutia riziki, lakini kuna watu ambao wapo vijijini kwetu hawapendi kabisa kuona wewe uko mjini ukijitafutia riziki kwaajili ya maisha yako. 
Watu hawa wamekuwa na tabia mbaya ya kutaka kuwaharibia watu walioko mijini ili maisha yao yawe ya ovyo. Utakuta watu hawa wakikunenea maneno mabaya na wengine kukuloga na hatima yake utajikuta huwezi kujenga nyumba nzuri na ukijenga nyumba nzuri kwaajili ya wazazi wako wanakuua au baba yako anauliwa au mama yako uliyemjengea hiyo nyumba anauawa kwa nguvu za giza kabla hajahamia kwenye hiyo nyumba. 
Wanachotaka wao ni kuona wazazi wako hawapati raha kutokana na matunda ya mtoto wao au wasionje kitu kinaitwa “FURAHA” katika maisha yao. Lakini leo tunatengua kila manuizo ya wanakijiji ambao ni wachawi, wenye wivu, wanaowaharibu maisha ya watu waishio mijini. Kila wanachokifanya kibaya kikawarudie wao kwa jina la Yesu Kristo.

Utakuta kijijini kwako wale wabaya wasiopenda maendeleo yako wakisema, “Mtoto huyu hatainuka tena, hatapata cheo tena, hatarudi kijijini akiwa mzima tena bali yatarudi maiti, hataolewa huko mjini na atakaa huko huko bila mume.” Leo tunatengua manuizo yao na tunavunja kila madhabahu uliyonenewa maneno mabaya kutoka kijijini kwako. Ni lazima madhabahu ivunjike, lazima mwaka 2019 utoboze, upate mpenyo, upate kuendelea mbele kwa kishindo kwa jina la Yesu Kristo.

Hukuvuka mwaka 2018 kuingia 2019 kwa bahati mbaya bali ni mpango wa Mungu wa kukuvusha katika mwaka wa Ongezeko na Mafanikio.

Shetani alichokosea ni kukuruhusu uvuke mwaka 2018 na kuingia mwaka wa mafanikio na ongezeko wa 2019. Madam umevuka 2018 na kuingia 2019 kila kamba na minyororo iliyokufungwa usifanikiwe mwaka 2019 tunaikata kwa jina la Yesu Kristo, maadam umevuka kuingia 2019 kila milango yako iliyofungwa usifikie ndoto zako za mwaka 2019 tunaifungua kwa jina la Yesu. Furaha utaiona kwa Jina la Yesu, Baraka za Mungu utaziona kwa jina la Yesu. 
Mungu atafanya njia pasipo na njia, Mungu atakutendea muujiza, yaliyo magumu yatakuwa mepesi kwa jina la Yesu Kristo. Huu ni mwaka wako wa mafanikio. Kila utakalolifanya litaenda kupata kibali na utatoboza kwa Jina la Yesu. Huu sio mwaka wa kuonewa na watu ambao huwajawatendea makosa, huu sio mwaka wa watu kula jasho lako bali ni mwaka wa maongezeko katika shughuli zako za kila siku na kila utakachokifanya kitapa kibali mbele za watu na mbele za Mungu.

Huu ni mwaka wako wa kufanikiwa. Umeteseka sana miaka ya nyuma lakini mwaka huu 2019 utakuwa mwaka wako wa kuvuka, kutoboza, kusafiri, kupata cheo, mafanikio na kutimiza ndoto zako. Unachotakiwa kufanya ni kukaa vizuri na Mungu kwa kufuata maagizo yake kupitia maandiko matakatifu na pia kuwasikiliza watumishi wa Mungu na kuwatii. 
Unapokuwa karibu na Mungu wako hakuna baya litakalokudhuri kwasababu unakuwa na ulizi wa kutosha kutoka kwa Mungu. watu wengi wanaangamia kwasababu wako mbali na Mungu, hawamtumikii Mungu, hawana uaminifu kwa Mungu, wanamuweka Mungu kama “Second option”.

Kama utakuwa mbali na Mungu na hufuati maagizo yake basi mabaya yatakuandama. Unatakiwa kutenda mema na kuacha mabaya yote. Mungu akusaidie mwaka huu uwe ni mwaka wako wa kuwa karibu na Mungu na utaona huruma za Mungu juu ya maisha yako.

BONYEZA HAPA KUONA VIDEO: https://www.youtube.com/watch?v=o_9RnZXJmDY&feature=youtu.be

-------

Mhubiri: Bishop Dr. Gertrude Rwakatare.

Mahali: Mlima wa Moto Mikocheni "B"

Tarehe: Jumapili 06.01.2019

Ibada ya Kupelekea maombi yetu na mahitaji yetu kwa Mungu






































Comments