15.10.2017: JACKSON BENTY ALIVYOMTUKUZA MUNGU SIKU YA JUMAPILI

Ilikuwa ni siku ya furaha sana kwa wana Mlima wa Moto Mikocheni "B" pale waliposikia sauti ya mtumishi wa Mungu Jackson Benty katika madhabahu ya miujiza ya Mlima wa Moto Mikocheni "B". Mwimbaji huyu alishangazwa sana kuona maendeleo ya kanisa la Mlima wa Moto Mikocheni "B" kwani ni miaka zaidi ya 8 hajawahi kukanyaga madhabahu ya Mlima wa Moto Mikocheni "B" kutokana na majukumu aliyokuwa nayo ya kihuduma mkoani Arusha na mataifa mbalimbali. Pia alipatwa na msiba mkubwa sana wa kufiwa na mke wake aliyepata ajali ya pikipiki mkoani Arusha.

Kanisa lilibarikiwa sana na uimbaji wa Jackson Benty siku ya Jumapili 15.10.2017 ya ibada ya KUVUNJA NGUVU ZA UCHAWI NA UGANGA kwa ujumbe mzito wenye kuelimisha, kuadibisha, kufundisha na kufariji.

Sasa naomba nikukaribishe wewe ambaye hujawahi kufika katika ibada zetu za Mlima wa Moto Mikocheni "B" na wewe ambaye kila Jumapili tunakuwa wote ndani ya nyumba ya BWANA.

Katika ibada zetu tunamuona Mungu katika maisha yetu. Maisha yetu ni mfano mkubwa wa ushuhuda wa matendo makuu ya Mungu. Kila kukicha, Mungu wetu anatufanya watu wapya.

Kuna baadhi ya watu walikuja wakiwa wamechoka mbaya kimwili na kiroho lakini walipokutana na Nguvu za Mungu kupitia mtumishi wake Bishop Dr. Gertrude Rwakatare, mambo yao yamenyooka kimwili na kiroho. Afya zao zimeimarika, uchumi wao umeongezeka, imani yao imeongezeka, hofu ya Mungu imewajaa, bidii ya kumtafuta Mungu imeongezeka.

Unapokuja kanisani unajifunza mambo mengi sana kupitia watumishi wa Mungu, na unatiwa moyo na kufarijiwa kutoka kwa waimbaji wenyeji na waimbaji wageni wanaofika kuabudu nasi. Kupitia nyimbo zao watu wanafunguliwa na kupokea kitu kipya katika maisha yao.

Jumapili hii tuliona Mungu akigusa maisha ya watu kupitia mwimbaji wa kimataifa Jackson Betty. Baadhi ya watu walitokwa na machozi kutokana na nyimbo yake iliyojaa nguvu za Mungu.

Karibuni Jumapili hii Mlima wa Moto Mikocheni "B". Ibada itaanza saa 3 asubuhi hadi saa 8 mchana. Usafiri ni bure kuanzia kituo cha mabasi cha Makumbusho au Mwenge kwenye mataa barabara ya Coca Cola DSM Tanzania. Ubarikiwe.

Jackson Benty








Comments